1 Sam. 10:20-27 Swahili Union Version (SUV)

20. Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa.

21. Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana.

22. Basi wakazidi kumwuliza BWANA, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye BWANA akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo.

23. Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu.

24. Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na BWANA, ya kuwa hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi!

25. Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za BWANA. Samweli akawaruhusu watu wote, waende kila mtu nyumbani kwake.

26. Sauli naye akaenda nyumbani kwake huko Gibea; na pamoja naye wakaenda kikosi cha watu, ambao Mungu alikuwa ameigusa mioyo yao.

27. Walakini wengine wasiofaa kitu wakasema, Huyu je! Atatuokoaje? Nao wakamdharau, wasimletee zawadi.

1 Sam. 10