18. akawaambia wana wa Israeli, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea;
19. lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za BWANA, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu.
20. Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa.
21. Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana.
22. Basi wakazidi kumwuliza BWANA, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye BWANA akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo.
23. Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu.