15. Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje?
16. Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo.
17. Basi Samweli akawakusanya watu mbele za BWANA huko Mispa
18. akawaambia wana wa Israeli, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea;
19. lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za BWANA, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu.
20. Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa.
21. Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana.
22. Basi wakazidi kumwuliza BWANA, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye BWANA akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo.