1 Sam. 10:1-17 Swahili Union Version (SUV)

1. Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! BWANA hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake.

2. Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu?

3. Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai;

4. nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao.

5. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri;

6. na roho ya BWANA itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.

7. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.

8. Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya.

9. Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile.

10. Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao.

11. Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

12. Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n’nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

13. Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu.

14. Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli.

15. Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje?

16. Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo.

17. Basi Samweli akawakusanya watu mbele za BWANA huko Mispa

1 Sam. 10