1 Nya. 9:20-34 Swahili Union Version (SUV)

20. naye Finehasi, mwana wa Eleazari, alikuwa mkuu wao hapo zamani, naye BWANA alikuwa pamoja naye.

21. Zekaria, mwana wa Meshelemia, alikuwa bawabu mlangoni pa ile hema ya kukutania.

22. Hao wote waliochaguliwa kuwa wangojezi wa malango walikuwa watu mia mbili na kumi na wawili. Nao wakahesabiwa kwa nasaba katika vijiji vyao, ambao Daudi na Samweli, huyo mwonaji, walikuwa wamewaweka katika kazi yao waliyoamaniwa.

23. Basi watu hao na wana wao walikuwa na usimamizi wa malango ya nyumba ya BWANA, yaani, nyumba ya maskani, kwa zamu.

24. Hao wangojezi walikuwapo pande zote nne, kuelekea mashariki, na magharibi, na kaskazini, na kusini.

25. Na ndugu zao, katika vijiji vyao, wakaamaniwa kuingia kila siku ya saba, zamu kwa zamu, ili kuwa pamoja nao;

26. kwa maana wale wangojezi wanne, waliokuwa wakuu, nao ni Walawi, walikuwa na kazi ya kuamaniwa, tena walikuwa juu ya vyumba na juu ya hazina katika nyumba ya Mungu.

27. Nao wakalala kandokando nyumbani mwa Mungu, kwa kuwa ulinzi wake ulikuwa juu yao, nayo ilikuwa kazi yao kuyafungua malango asubuhi baada ya asubuhi.

28. Na baadhi yao walikuwa na ulinzi wa vyombo vya huduma; kwani huingizwa kwa hesabu, na kutolewa kwa hesabu vile vile.

29. Na baadhi yao waliamaniwa kuviangalia vyombo vya nyumbani, na vyombo vyote vya Patakatifu; na kuwa juu ya unga safi, na divai, na mafuta, na ubani, na manukato.

30. Na baadhi ya wana wa makuhani waliweka tayari machanganyiko ya manukato.

31. Naye Matithia, Mlawi mmojawapo, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Shalumu, Mkora, aliamaniwa kazi ya kuviangalia vitu vile vilivyookwa kaangoni.

32. Na baadhi ya ndugu zao, wa wana wa Wakohathi, walikuwa juu ya mikate ile ya Wonyesho, ili kuiandaa kila sabato.

33. Tena hawa ndio waimbaji, wakuu wa mbari za baba zao katika Walawi, ambao walikaa vyumbani, kisha walikuwa hawana kazi nyingine; kwa kuwa walitumika katika kazi yao mchana na usiku.

34. Hao walikuwa wakuu wa mbari za baba zao katika Walawi, katika vizazi vyao vyote, watu wakuu; nao walikuwa wakikaa huko Yerusalemu.

1 Nya. 9