7. Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo.
8. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la BWANA, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za BWANA, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele.
9. Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.
10. Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.
11. Ndipo Daudi akampa Sulemani mwanawe mfano wa ukumbi wa hekalu, na nyumba zake, na hazina zake, na orofa zake, na vyumba vyake vya ndani, na mahali pa kiti cha rehema;
12. na mfano wa yote aliyokuwa nayo kwa roho, katika habari ya nyua za nyumba ya BWANA, na ya vyumba vyote vilivyoizunguka, ya hazina za nyumba ya Mungu, na ya hazina za vitu vilivyowekwa wakfu;
13. tena katika habari ya zamu za makuhani na Walawi, na ya kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya BWANA, na ya vyombo vyote vya utumishi nyumbani mwa BWANA;