10. Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.
11. Ndipo Daudi akampa Sulemani mwanawe mfano wa ukumbi wa hekalu, na nyumba zake, na hazina zake, na orofa zake, na vyumba vyake vya ndani, na mahali pa kiti cha rehema;
12. na mfano wa yote aliyokuwa nayo kwa roho, katika habari ya nyua za nyumba ya BWANA, na ya vyumba vyote vilivyoizunguka, ya hazina za nyumba ya Mungu, na ya hazina za vitu vilivyowekwa wakfu;
13. tena katika habari ya zamu za makuhani na Walawi, na ya kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya BWANA, na ya vyombo vyote vya utumishi nyumbani mwa BWANA;
14. ya dhahabu kwa uzani kwa vyombo vya dhahabu, kwa vyombo vyote vya utumishi wa kila namna; ya fedha kwa uzani kwa vyombo vyote vya fedha, kwa vyombo vyote vya utumishi wa kila namna;
15. kwa uzani tena kwa vinara vya dhahabu, na kwa taa zake za dhahabu, kwa uzani, kwa kila kinara, na kwa taa zake; na kwa vinara vya fedha, kwa uzani kwa kila kinara na kwa taa zake, kwa kadiri ya matumizi ya kila kinara;
16. na dhahabu kwa uzani kwa meza za mikate ya wonyesho, kwa kila meza; na fedha kwa meza za fedha;
17. na nyuma, na mabakuli, na vikombe vya dhahabu safi; na kwa matasa ya dhahabu, kwa uzani kwa kila tasa; na kwa matasa ya fedha, kwa uzani kwa kila tasa;
18. na kwa madhabahu ya kufukizia, dhahabu iliyosafika sana kwa uzani; na dhahabu kwa mfano wa gari, yaani, makerubi, yenye kutandaza mabawa, na kulifunika sanduku la agano la BWANA.
19. Hayo yote, akasema Daudi, yamenielea kwa maandiko kutoka kwa mkono wa BWANA, naam, kazi zote za mfano huu.