8. Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.
9. Wakatoka wana wa Amoni, wakapanga vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwandani.
10. Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami.
11. Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni.
12. Akasema, Wakiwa Washami ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe.
13. Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake.
14. Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake.
15. Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu.
16. Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakapeleka wajumbe, wakawavuta Washami walioko ng’ambo ya Mto, na Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza.
17. Alipoambiwa Daudi; akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akawajia, akapanga vita juu yao. Basi Daudi alipopanga vita juu ya Washami, wakapigana naye.
18. Washami wakakimbia mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami watu wa magari saba elfu, na askari waendao kwa miguu arobaini elfu, akamwua na Shobaki, jemadari wa jeshi.
19. Na watumwa wa Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Daudi, wakamtumikia; wala Washami hawakukubali kuwasaidia wana wa Amoni tena.