1. Ikawa, Daudi alipokuwa akikaa nyumbani mwake, Daudi akamwambia nabii Nathani, Angalia, mimi ninakaa katika nyumba ya mwerezi, bali sanduku la agano la BWANA linakaa chini ya mapazia.
2. Naye Nathani akamwambia Daudi, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; kwa maana Mungu yu pamoja nawe.
3. Ikawa usiku uo huo, neno la Mungu likamjia Nathani, kusema,
4. Nenda, kamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa;
5. kwa maana sikukaa ndani ya nyumba tangu siku ile nilipowaleta Israeli huku hata leo; lakini hema kwa hema nimehamia, na maskani kwa maskani.