1 Nya. 15:11-23 Swahili Union Version (SUV)

11. Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu,

12. akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari.

13. Kwani kwa sababu ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, BWANA, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta sawasawa na sheria.

14. Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli.

15. Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la BWANA.

16. Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha.

17. Basi Walawi wakamwagiza Hemani mwana wa Yoeli; na wa nduguze, Asafu mwana wa Berekia; na wa wana wa Merari ndugu zao, Ethani mwana wa Kishi;

18. na pamoja nao ndugu zao kwa cheo cha pili, Zekaria, na Yaasieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu; na Benaya, na Maaseya, na Matithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, mabawabu.

19. Hivyo hao waimbaji, Hemani, Asafu, na Ethani, wakaagizwa kupiga matoazi yao ya shaba kwa sauti kuu;

20. na Zekaria, na Yaasieli na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu, na Maaseya, na Benaya, wenye vinanda vya sauti ya Alamothi;

21. na Matithiya, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, na Azazia, wenye vinubi vya sauti ya Sheminithi,

22. waongoze. Na Kenania, mkuu wa Walawi, alikuwa juu ya uchukuzi; yeye aliusimamia uchukuzi, kwa sababu alikuwa mstadi.

23. Na Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.

1 Nya. 15