1. Basi Daudi akajifanyia nyumba katika mji wa Daudi; akapaweka tayari mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema.
2. Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua BWANA, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima.
3. Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la BWANA, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari.
4. Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi;
5. wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia na ishirini;
6. wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini;
7. wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia na thelathini;
8. wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili;
9. wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini;
10. wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia na kumi na wawili.
11. Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu,
12. akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari.