1 Kor. 7:5-17 Swahili Union Version (SUV)

5. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.

6. Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.

7. Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.

8. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.

9. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.

10. Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;

11. lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.

12. Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.

13. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.

14. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.

15. Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.

16. Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?

17. Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote.

1 Kor. 7