8. na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.
9. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu.
10. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.
11. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
12. Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu?
13. Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka;
14. tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure.
15. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.
16. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka.
17. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu.
18. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea.
19. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.
20. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.