22. Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini lakini kuhutubu si kwa ajili yao wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio.
23. Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu?
24. Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote;
25. siri za moyo wake huwa wazi; na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudifudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka.
26. Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.
27. Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.
28. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.
29. Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.
30. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.
31. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe.