1 Kor. 10:10-22 Swahili Union Version (SUV)

10. Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.

11. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

12. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.

13. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.

14. Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.

15. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.

16. Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?

17. Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

18. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?

19. Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?

20. Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.

21. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.

22. Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?

1 Kor. 10