1 Fal. 8:50-58 Swahili Union Version (SUV)

50. ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia.

51. Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuu ya chuma.

52. Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia.

53. Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU.

54. Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni.

55. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema,

56. Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake.

57. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe;

58. aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu.

1 Fal. 8