1 Fal. 8:18-33 Swahili Union Version (SUV)

18. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako.

19. Lakini wewe hutanijengea nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.

20. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.

21. Na humo sanduku hili nimelifanyizia mahali, ambalo ndani yake mna maagano ya BWANA, aliyoyafanya na baba zetu, hapo alipowatoa katika nchi ya Misri.

22. Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni.

23. Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote.

24. Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.

25. Na sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda.

26. Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu.

27. Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!

28. Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee BWANA, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo.

29. Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa.

30. Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.

31. Ikiwa mtu amemkosa mwenzake, na kupewa sharti ya kiapo aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako, katika nyumba hii;

32. basi, usikie huko mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimpatiliza mtu mbaya, kwa kuleta njia yake juu ya kichwa chake; na kumpa mwenye haki haki yake, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.

33. Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea tena kwako, na kulikiri jina lako wakikuomba na kukusihi katika nyumba hii;

1 Fal. 8