1. Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya kutoka wana wa Israeli katika nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya BWANA.
2. Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea BWANA, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini.
3. Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba.
4. Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia.
5. Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kote kote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote.
6. Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba.
7. Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba.
8. Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kuume wa nyumba; mtu hupanda madaraja ya kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu.
9. Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi.