1. Huyo Sulemani akafanya ujamaa na Farao, mfalme wa Misri, akamwoa binti yake Farao, akamleta mjini mwa Daudi, hata alipokwisha kuijenga nyumba yake, na nyumba ya BWANA, na ukuta wa kuuzunguka Yerusalemu.
2. Ila watu walikuwa wakichinja dhabihu katika mahali pa juu, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la BWANA, hata siku zile.
3. Sulemani naye akampenda BWANA, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
4. Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile.
5. Na huko Gibeoni BWANA akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.