24. Basi kwa hiyo, BWANA aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia.
25. Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.
26. Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Enenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu.
27. Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo.