2. Neno la BWANA likamjia, kusema,
3. Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.
4. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.
5. Basi akaenda akafanya kama alivyosema BWANA; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani.
6. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.
7. Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.
8. Neno la BWANA likamjia, kusema,
9. Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.
10. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.
11. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.
12. Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.
13. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.
14. Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi.
15. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.
16. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya.