1 Fal. 15:18-31 Swahili Union Version (SUV)

18. Ndipo Asa akazitwaa fedha zote na dhahabu zilizosalia katika hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akazitia mikononi mwa watumishi wake; mfalme Asa akawatuma kwa Ben-hadadi, mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,

19. Tumepatana mimi nawe, na baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea zawadi, fedha na dhahabu; basi nenda, uyavunje mapatano yako na Baasha mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.

20. Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawatuma wakuu wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli, akapiga Iyoni, na Dani, na Abel-beth-maaka na Kinerothi yote, na nchi yote ya Naftali.

21. Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo akaacha kuujenga Rama, akaenda akakaa Tirza.

22. Ndipo mfalme Asa akatangaza kwa Yuda pia; asiachiliwe mtu; nao wakayachukua mawe ya Rama na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye mfalme Asa akajenga kwa vitu hivyo Geba wa Benyamini na Mispa.

23. Na mambo yote ya Asa yaliyosalia, na nguvu zake zote, na yote aliyoyafanya, na miji aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Lakini alipokuwa mzee alikuwa na ugonjwa wa miguu.

24. Asa akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake.

25. Nadabu mwana wa Yeroboamu alianza kutawala juu ya Israeli, mwaka wa pili wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala juu ya Israeli miaka miwili.

26. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya baba yake, na kosa lake alilowakosesha Israeli.

27. Basi Baasha wa Ahiya, wa mbari ya Isakari, akamfanyia fitina; Baasha akampiga huko Gibethoni ulio wa Wafilisti; kwani Nadabu na Israeli wote walikuwa wakiuhusuru Gibethoni.

28. Mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda Baasha akamwua, akatawala mahali pake.

29. Ikawa mara alipotawala, akawapiga nyumba yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu mwenye pumzi ye yote, hata alipomharibu sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mtumishi wake Ahiya, Mshiloni;

30. kwa sababu ya makosa yake Yeroboamu aliyoyakosa, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; kwa sababu ya chukizo lake alilomchukiza BWANA, Mungu wa Israeli, hata kumghadhibisha.

31. Basi mambo yote ya Nadabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

1 Fal. 15