13. Hata na Maaka, mamaye, akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.
14. Lakini mahali pa juu hapakuondoshwa; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu kwa BWANA siku zake zote.
15. Akavileta vile vitu alivyovitakasa baba yake, na vile alivyovitakasa yeye mwenyewe, katika nyumba ya BWANA, fedha; na dhahabu, na vyombo.
16. Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.
17. Kisha, Baasha mfalme wa Israeli akaondoka juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.
18. Ndipo Asa akazitwaa fedha zote na dhahabu zilizosalia katika hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akazitia mikononi mwa watumishi wake; mfalme Asa akawatuma kwa Ben-hadadi, mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,