1 Fal. 11:3-14 Swahili Union Version (SUV)

3. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.

4. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.

5. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni.

6. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.

7. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni.

8. Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.

9. Basi BWANA akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha BWANA, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,

10. akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru BWANA.

11. Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.

12. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.

13. Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.

14. Ndipo BWANA akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; yeye alikuwa wa wazao wake mfalme wa Edomu.

1 Fal. 11