6. Tena baba yake hakumchukiza wakati wo wote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu.
7. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata.
8. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia.
9. Adonia akachinja kondoo, na ng’ombe, na vinono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Rogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme;
10. ila Nathani, nabii, na Benaya, na mashujaa, na Sulemani nduguye, hakuwaita hao.
11. Ndipo Nathani akamwambia Bath-sheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, anamiliki, na bwana wetu Daudi hana habari?
12. Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani.
13. Enenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia?