Yoshua 6:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Kulingana na amri ya Yoshua, wale makuhani saba waliokuwa na mabaragumu saba ya kondoo dume wakaenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakiwa wanapiga mabaragumu, nyuma yao wakifuatwa na lile sanduku la agano.

9. Wale watu wenye silaha wakawatangulia wale makuhani ambao walikuwa wanapiga mabaragumu, na walinzi wengine wakifuata nyuma ya sanduku hilo, huku mabaragumu yakilia kwa mfululizo.

10. Lakini Yoshua akawaamuru watu, “Msipige kelele au kutoa sauti, wala neno lolote lisitoke vinywani mwenu, mpaka siku ile ambapo nitawaambieni mpige kelele; wakati huo ndipo mtakapopiga kelele.”

11. Basi, Yoshua aliwafanya wale watu wauzunguke mji mara moja kila siku wakiwa wamebeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu na kurudi kambini kulala usiku.

12. Asubuhi yake Yoshua akaamka alfajiri na mapema, na makuhani wakalibeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.

13. Wale makuhani saba wenye mabaragumu saba za kondoo dume walitembea mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu wakipiga mabaragumu mfululizo. Watu wenye silaha walilitangulia sanduku la Mwenyezi-Mungu na walinzi wengine nyuma yake. Mabaragumu yakaendelea kupigwa.

14. Siku ya pili yake waliuzunguka huo mji mara moja; na kurudi tena kambini kwao. Walifanya hivyo kwa muda wa siku sita.

Yoshua 6