26. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua watu hao na kuwapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla.
27. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi.Basi, watu wa Yuda walikwenda uhamishoni nje ya nchi yao.
28. Ifuatayo ni idadi ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua uhamishoni mnamo mwaka wa saba wa utawala wake: Alichukua Wayahudi 3,023;
29. mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, alichukua kutoka Yerusalemu mateka 832;
30. mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Nebukadneza, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alichukua mateka Wayahudi 745. Jumla ya mateka wote ilikuwa watu 4,600.
31. Mnamo mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda alipopelekwa uhamishoni, siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, mwaka uleule alipofanywa mfalme, alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.
32. Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye uhamishoni huko Babuloni.