17. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba nyeusi ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na vikalio na birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi yote mpaka Babuloni.
18. Kadhalika, walichukua vyungu, sepetu, mikasi, makarai, vijiko vikubwa na vyombo vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu.
19. Pia kapteni wa walinzi wa mfalme alichukua vibakuli, vyetezo, mabirika, vyungu, vinara vya taa, vijiko vikubwa na mabakuli ya sadaka za vinywaji, vyombo hivyo vikiwa vya dhahabu au vya fedha.
20. Kuhusu vitu Solomoni alivyotengeneza: Nguzo mbili, birika kubwa moja na sanamu za fahali kumi na mbili za shaba nyeusi ambazo zilikuwa chini ya hilo birika kubwa pamoja na vikalio, shaba nyeusi ya vitu hivi vyote ilikuwa na uzito mwingi sana.
21. Kila moja ya nguzo hizo mbili ilikuwa na urefu wa mita 8, mzingo wake mita 5.25, na unene wa milimita 75, zote zilikuwa wazi ndani.
22. Juu ya kila nguzo kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi; urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 2 na sentimita 20. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya wavu ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi.
23. Kulikuwa na makomamanga tisini na sita ubavuni mwa nguzo hizo; jumla ya makomamanga yote ilikuwa 100 na mapambo kandokando yake.
24. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, na Sefania kuhani wa pili, pamoja na walinda mlango watatu;
25. na kutoka mjini alimchukua ofisa mmoja ambaye alikuwa akiongoza askari vitani, pamoja na watu saba washauri wa mfalme ambao aliwakuta mjini. Kadhalika alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu mashuhuri sitini ambao aliwakuta mjini Yerusalemu.
26. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua watu hao na kuwapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla.
27. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi.Basi, watu wa Yuda walikwenda uhamishoni nje ya nchi yao.
28. Ifuatayo ni idadi ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua uhamishoni mnamo mwaka wa saba wa utawala wake: Alichukua Wayahudi 3,023;
29. mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, alichukua kutoka Yerusalemu mateka 832;
30. mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Nebukadneza, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alichukua mateka Wayahudi 745. Jumla ya mateka wote ilikuwa watu 4,600.
31. Mnamo mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda alipopelekwa uhamishoni, siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, mwaka uleule alipofanywa mfalme, alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.
32. Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye uhamishoni huko Babuloni.
33. Basi, Yehoyakini alibadili mavazi yake ya kifungoni, akawa anapata chakula chake daima mezani kwa mfalme.