Yeremia 43:5-13 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Hapo Yohanani mwana wa Karea na makamanda wote wa majeshi waliwachukua watu wote wa Yuda waliosalia ambao walikuwa wamerudi nchini Yuda kutoka mataifa yote ambako walikuwa wametawanywa;

6. wanaume, wanawake, watoto, binti za mfalme na kila mtu ambaye Nebuzaradani, kapteni wa walinzi, alikuwa amemwachia Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, wakamchukua pia nabii Yeremia na Baruku mwana wa Neria,

7. wakaenda nchini Misri, wakawasili mjini Tahpanesi. Ndivyo walivyokataa kutii alichosema Mwenyezi-Mungu

8. Basi neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia huko Tahpanesi:

9. “Chukua mawe makubwa, ukayafiche katika chokaa ya matofali kwenye lango la ikulu ya Farao mjini Tahpanesi, watu wa Yuda wakiwa wanaona.

10. Kisha waambie hivi: Tazameni mimi nitamtuma na kumleta Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, mtumishi wangu, naye ataweka kiti chake cha enzi juu ya mawe haya ambayo nimeyaficha hapa, na kutandaza paa la kifalme juu yake.

11. Atakapofika ataiangamiza nchi ya Misri. Hapo waliopangiwa kufa kwa maradhi watakufa kwa maradhi, waliopangiwa kuchukuliwa mateka, watachukuliwa mateka; waliopangiwa kufia vitani watafia vitani.

12. Mimi nitawasha moto katika mahekalu ya miungu ya Misri; naye Nebukadneza ataiteketeza miungu hiyo kwa moto au kuichukua mateka mpaka Babuloni. Ataisafisha nchi ya Misri kama mchungaji atoavyo kupe katika vazi lake na kuondoka Misri akiwa mshindi.

13. Ataivunja minara ya ukumbusho iliyoko huko Heliopoli nchini Misri, na mahekalu ya miungu ya Misri atayateketeza kwa moto.”

Yeremia 43