Ufunuo 9:4-15 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso.

5. Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na nge.

6. Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.

7. Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.

8. Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.

9. Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani.

10. Walikuwa na mikia na miiba kama nge, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano.

11. Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani Mwangamizi.

12. Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.

13. Kisha, malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu.

14. Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Eufrate!”

15. Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanadamu.

Ufunuo 9