Ufunuo 18:3-14 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo.”

4. Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema,“Watu wangu, ondokeni kwake,ili msishirikiane naye katika dhambi zake,msije mkaipata adhabu yake.

5. Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno,zimerundikana mpaka mbinguni,na Mungu ameyakumbuka maovu yake.

6. Mtendeeni kama alivyowatendea nyinyi;mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda.Mchanganyieni kikombeni mwake kinywaji kikali maradufu.

7. Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake,kulingana na kuishi kwake kwa anasa.Maana anajisemea moyoni: ‘Ninaketi hapa; mimi ni malkia.Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!’

8. Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja:Ugonjwa, huzuni na njaa.Atachomwa moto,maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ana nguvu.”

9. Wafalme wa dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea.

10. Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake na kusema, “Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata.”

11. Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao;

12. hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marumaru;

13. mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng'ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu.

14. Wafanyabiashara wanamwambia: “Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!”

Ufunuo 18