1. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Nisikilizeni enyi mnaotaka kukombolewa,nyinyi mnaonitafuta mimi Mwenyezi-Mungu.Utazameni mwamba mlimochongwa,chimbo la mawe mlimochimbuliwa.
2. Mkumbukeni Abrahamu babu yenu,na Sara aliyewazaa nyinyi.Abrahamu alikuwa hana mtoto wakati nilipomwita,lakini nilimbariki na kumfanya kuwa na wengi.
3. “Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji mji wa Siyoni,nitaparekebisha mahali pake pote palipoharibika.Nyika zake nitazifanya kama bustani ya Edeni,majangwa yake kama bustani ya Mwenyezi-Mungu.Kwake kutapatikana furaha na shangwe,na nyimbo za shukrani zitasikika humo.
4. “Nisikilizeni enyi watu wangu,nitegeeni sikio enyi taifa langu.Sheria na haki zitatoka kwangu mimi;nazo zitakuwa mwanga wa mataifa.
5. Nitaleta ukombozi hima;wokovu nitakaoleta waanza kutokea.Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa.Wakazi wa nchi za mbali wananingojea,wanaitegemea nguvu yangu.
6. Inueni macho mzitazame mbingu,kisha tazameni dunia huko chini.Mbingu zitatoweka kama moshi,dunia itachakaa kama vazi,na wakazi wake watakufa kama wadudu.Lakini wokovu niuletao wadumu milele;ukombozi wangu kamwe hautakoma.