10. Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira siku hiyo, akaapa akisema,
11. ‘Hakika hakuna mtu yeyote kati ya watu waliotoka Misri mwenye umri wa miaka ishirini na zaidi atakayeiona nchi niliyoapa kuwapa Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwa sababu hawakunitii kikamilifu.’
12. Wote hawataiona, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, maana wao wamenitii kikamilifu.
13. Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira dhidi ya Waisraeli, akawafanya watangetange jangwani kwa muda wa miaka arubaini; kizazi kizima kilichokuwa kimefanya maovu mbele yake kikafariki.
14. Na sasa, enyi kizazi cha wenye dhambi, mmezuka mahali pa wazee wenu, kuongeza tena hasira kali ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Waisraeli.
15. Kama nyinyi mkikataa kumfuata, yeye atawaacheni tena jangwani, nanyi mtasababisha watu hawa wote waangamie.”
16. Basi, wakamwendea Mose, wakamwambia, “Kwanza turuhusu tuwajengee kondoo wetu mazizi, na watoto wetu miji hapa.
17. Lakini sisi wenyewe tutachukua silaha zetu tayari kwenda vitani pamoja na ndugu zetu Waisraeli, na tutakuwa mstari wa mbele vitani hadi tuwafikishe mahali watakapokaa. Wakati huo watoto wetu watakaa kwenye miji yenye ngome, ili kujilinda na wenyeji wa nchi hii.
18. Hatutarudi nyumbani hadi hapo Waisraeli wengine wote watakapomiliki maeneo yao waliyogawiwa.
19. Hatutamiliki mali yoyote miongoni mwao ngambo ya mto Yordani, kwa sababu sisi tumepata maeneo yetu ngambo hii, mashariki ya mto Yordani.”
20. Mose akawaambia, “Kama kweli mtafanya kama mlivyosema, basi papa hapa mbele ya Mwenyezi-Mungu, chukueni silaha zenu kwenda vitani.
21. Kila mpiganaji wenu atavuka mto Yordani na mkiwa chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mtawashambulia adui zetu mpaka Mwenyezi-Mungu awashinde,
22. na kuimiliki nchi. Mkisha fanya hayo, mtarudi, maana mtakuwa mmetimiza wajibu wenu kwa Mwenyezi-Mungu na ndugu zenu Waisraeli. Kisha Mwenyezi-Mungu atakubali nchi hii ya mashariki ya Yordani kuwa mali yenu.
23. Lakini nawaonyeni kwamba msipotimiza ahadi yenu, mtakuwa mnamtendea Mwenyezi-Mungu dhambi; jueni kwa hakika kwamba mtaadhibiwa.
24. Wajengeeni watoto wenu miji na kondoo wenu mazizi; lakini fanyeni kama mlivyoahidi.”
25. Kisha, watu wa Gadi na wa Reubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama ulivyotuamuru.
26. Wake zetu, watoto wetu na kondoo na ng'ombe, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
27. Lakini sisi watumishi wako tuko tayari kwenda vitani chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu. Tutavuka mto Yordani na kupigana, kama ulivyosema.”
28. Basi, Mose akatoa amri zifuatazo kwa kuhani Eleazari, kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kwa viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli:
29. “Ikiwa watu wa Gadi na wa Reubeni watavuka mto Yordani pamoja nanyi wakiwa na silaha zao chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mkashinda na kuichukua nchi hiyo, basi mtawapa nchi ya Gileadi iwe mali yao.