22. Hasira ya Mungu iliwaka kwa sababu Balaamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akakabiliana naye njiani. Wakati huo Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa na watumishi wake.
23. Basi, punda alimwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Kwa hiyo aliiacha njia, akaenda pembeni. Balaamu akampiga huyo punda, akamrudisha njiani.
24. Kisha malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu akatangulia mbele, akasimama mahali penye njia nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili.
25. Punda alipomwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu, akajisukumiza ukutani na kuubana mguu wa Balaamu hapo. Kwa hiyo Balaamu akampiga tena huyo punda.
26. Kisha malaika akatangulia tena, akasimama mahali pembamba pasipo na nafasi ya kupita kulia wala kushoto.
27. Punda alipomwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, akalala chini. Balaamu akawaka hasira, akampiga kwa fimbo yake.
28. Hapo Mwenyezi-Mungu akakifunua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?”
29. Balaamu akamwambia punda, “Wewe umenidhihaki! Kama ningekuwa na upanga ningalikuulia mbali sasa hivi!”
30. Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote hadi siku hii ya leo? Je, nimewahi kukutendea namna hii?” Balaamu akajibu, “La.”
31. Hapo, Mwenyezi-Mungu akayafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Balaamu akajitupa chini kifudifudi.
32. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya.
33. Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.”
34. Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.”
35. Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Nenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia.” Basi, Balaamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki.
36. Balaki alipopata habari kwamba Balaamu anakuja, alitoka kwenda kumlaki mjini Ari, mji uliokuwa ukingoni mwa mto Arnoni kwenye mpaka wa Moabu.
37. Balaki akamwambia Balaamu, “Kwa nini hukuja kwangu mara moja nilipokuita? Je, ulifikiri sitaweza kukutunukia heshima ya kutosha?”