Ezekieli 34:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Kondoo waliopotea nitawatafuta na waliotangatanga nitawarudisha nyumbani. Waliojeruhiwa nitawatibu, na wale walio dhaifu nitawapa nguvu. Kondoo wanono na wenye nguvu nitawaangamiza. Mimi nitawachunga kondoo kama itakiwavyo.

17. “Na Nyinyi mlio kundi langu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaamua baina ya kondoo na kondoo; baina ya kondoo dume na mbuzi.

18. Baadhi yenu mnakula malisho mazuri na pia kukanyagakanyaga yale yaliyobaki! Mnakunywa maji safi na yanayobaki mnayachafua kwa miguu yenu!

19. Je, kondoo wangu wengine wale malisho yaliyokanyagwakanyagwa na kunywa maji yaliyochafuliwa?

20. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Mimi mwenyewe nitaamua kati ya kondoo wanono na kondoo dhaifu.

21. Nyinyi mnawasukuma kwa mbavu na kwa mabega na kuwapiga pembe kondoo wote walio dhaifu mpaka mmewatawanya mbali na kundi.

22. Lakini mimi nitawaokoa kondoo wangu wasiwe tena mawindo. Nitatoa hukumu juu ya kila kondoo.

23. Nitamweka mchungaji mmoja juu yao, mfalme kama mtumishi wangu Daudi. Yeye atawalisha na kuwa mchungaji wao.

24. Nami Mwenyezi-Mungu, nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

25. Nitafanya nao agano la amani. Nitaondoa wanyama wakali katika nchi, ili kondoo wangu wakae mbugani kwa usalama na kulala msituni.

26. “Nitawafanya waishi kandokando ya mlima wangu mtakatifu na kuwabariki. Nitawaletea mvua kwa wakati wake, nazo zitakuwa mvua za baraka.

Ezekieli 34