26. “Watu wa Mesheki na wa Tabali wote wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Watu hao wote wasiomjua Mungu walikufa vitani, watu ambao walipokuwa hai walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
27. Hao wasiomjua Mungu hawakuzikwa pamoja na mashujaa wa kale, ambao walikwenda kuzimu kwa wafu wakiwa na silaha zao, mapanga yao chini ya vichwa vyao na ngao zao juu ya miili yao. Mashujaa hao walipokuwa wanaishi bado walijaza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
28. Basi, nyinyi Wamisri mtaangamizwa na kulazwa miongoni mwa wasiomjua Mungu waliouawa vitani.
29. “Waedomu wako huko pamoja na wafalme wao na wakuu wao wote. Walipokuwa bado hai walikuwa na nguvu sana, lakini sasa wamelazwa kwa wafu pamoja na wasiomjua Mungu waliouawa vitani.
30. “Viongozi wote wa watu wa kaskazini wako huko pia; hata Wasidoni wote walikwenda kujiunga na wafu. Walipokuwa bado wanaishi, walisababisha vitisho kwa nguvu zao, lakini sasa hao wasiomjua Mungu wamelazwa chini kwa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. Wanashiriki aibu ya wale walioshuka shimoni kwa wafu.
31. “Farao, atakapowaona hao wote atafarijika kwa ajili ya wingi wa majeshi yake yote; mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
32. Nilimfanya Farao aeneze vitisho katika nchi ya walio hai, lakini sasa yeye mwenyewe pamoja na jeshi lake lote watauawa vitani na kulazwa pamoja na wasiomjua Mungu, waliokufa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”