2. Basi neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:
3. “Wewe mtu, watu hawa wamekubali mioyo yao itawaliwe na sanamu za miungu; miungu hiyo inawaelekeza kutenda dhambi. Je, nitakubali kuulizwa nao shauri?
4. Basi, sema nao uwaambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli anayekubali sanamu za miungu zimtawale moyoni, na kuiruhusu miungu hiyo kumwelekeza kutenda dhambi, kisha akaja kumwomba shauri nabii, atapata jibu kutoka kwangu ambalo litazifaa hata sanamu zake nyingi za miungu.
5. Nitaigusa mioyo ya Waisraeli ili wanirudie, kwani wamejitenga mbali nami kwa kuabudu sanamu zao za miungu.
6. “Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tubuni, na kuacha kuziabudu sanamu zenu za miungu. Acheni kufanya machukizo.
7. Wakati wowote mmojawapo wa Waisraeli au mgeni yeyote akaaye katika Israeli, anapojitenga nami na kuanza kuziabudu sanamu za miungu kwa bidii na dhambi hiyo ikawa kizuizi kati yangu naye, halafu akamwendea nabii ili kujua matakwa yangu, basi, mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe, nitamjibu mtu huyo.
8. Nitapambana naye. Nitamfanya kuwa ishara na kielelezo; nitamwondoa kabisa kutoka taifa langu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
9. Na ikiwa nabii huyo atadanganyika akasema kitu, basi mimi Mwenyezi-Mungu nimempotosha. Nami nitanyosha mkono wangu kumwondoa nabii huyo kutoka kwa watu wangu wa Israeli.
10. Nitamwadhibu huyo nabii pamoja na huyo mtu aliyekuja kumwuliza matakwa yangu; wote watapata adhabu ileile,
11. ili watu wa Israeli wasiniache tena na kujichafua wenyewe kwa kutenda dhambi; ili wawe watu wangu nami niwe Mungu wao. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
12. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
13. “Wewe mtu! Taifa fulani likitenda dhambi kwa kukosa uaminifu kwangu, mimi nitanyosha mkono wangu kuliadhibu. Nitaiondoa akiba yake ya chakula na kuliletea njaa. Nitawaua watu na wanyama wake.
14. Hata kama Noa, Daneli na Yobu wangalikuwamo nchini humo, wangeyaokoa tu maisha yao wenyewe kwa uadilifu wao.
15. Tena nitapeleka wanyama wa porini katika nchi hiyo na kuwanyanganya watoto wao na kuifanya nchi hiyo kuwa ukiwa, hata hakuna mtu yeyote atakayeweza kupita nchini humo kwa sababu ya wanyama wakali.
16. Hata kama hao watu watatu mashuhuri wangalikuwamo nchini humo, naapa kwa jina langu, mimi Mwenyezi-Mungu, hawangeweza kuwaokoa watoto wao wenyewe; wao wenyewe tu wangeokolewa, lakini nchi hiyo ingekuwa ukiwa.