8. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa maneno yenu ni udanganyifu na maono yenu ni ya uongo mtupu, basi, mimi nitapambana nanyi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
9. Nitanyosha mkono wangu dhidi yenu nyinyi manabii mnaotoa maono ya uongo na kutabiri udanganyifu mtupu. Watu wangu watakapokutanika kuamua mambo, nyinyi hamtakuwapo. Wala hamtakuwa katika orodha ya watu wa Israeli na hamtaingia katika nchi ya Israeli; ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.
10. Manabii hao wanawapotosha watu wangu na kuwaambia ‘Kuna amani’, wakati hakuna amani. Watu wangu wanajenga ukuta usiofaa, nao wanaupaka chokaa!
11. Sasa waambie hao manabii wanaopaka chokaa ukuta huo kwamba itanyesha mvua kubwa ya mawe na dhoruba na ukuta huo utaanguka.
12. Je, utakapoanguka, watu hawatawauliza: ‘Na ile chokaa mlioupaka iko wapi?’
13. Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kwa ghadhabu yangu nitazusha upepo wa dhoruba na mvua nyingi ya mawe, navyo vitauangusha ukuta huo.