18. Pasaka kama hiyo ilikuwa haijasherehekewa katika Israeli yote tangu siku za nabii Samueli. Hapajatokea mfalme hata mmoja wa Israeli aliyeadhimisha Pasaka kama hii iliyoadhimishwa na mfalme Yosia pamoja na makuhani, Walawi na watu wote wa Yuda, watu wa Israeli na wakazi wa Yerusalemu.
19. Pasaka hiyo iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake mfalme Yosia.
20. Baada ya haya yote aliyofanya mfalme Yosia kwa ajili ya hekalu, Neko, mfalme wa Misri, aliongoza jeshi lake kwenda kushambulia Karkemishi kwenye mto Eufrate. Naye mfalme Yosia alitoka kumkabili,
21. lakini mfalme Neko akamtumia ujumbe usemao: “Vita hivi havikuhusu wewe hata kidogo ewe mfalme wa Yuda. Sikuja kupigana nawe bali dhidi ya maadui zangu, na Mungu ameniamuru niharakishe. Acha basi kumpinga Mungu, ambaye yu upande wangu, la sivyo atakuangamiza.”
22. Lakini Yosia hakukubali kumwachia. Alikataa kuyasikiliza maneno aliyonena Mungu kwa njia ya Neko, kwa hiyo akajibadilisha ili asitambulike, kisha akaingia vitani katika tambarare ya Megido.
23. Nao wapiga upinde walimpiga mshale mfalme Yosia; basi ndipo mfalme alipowaambia watumishi wake: “Niondoeni! Nimejeruhiwa vibaya sana.”
24. Watumishi wake walimtoa katika gari lake la farasi, wakambeba na gari lake la pili hadi Yerusalemu. Hapo akafariki dunia na kuzikwa katika makaburi ya kifalme. Watu wote wa Yuda na Yerusalemu waliomboleza kifo cha Yosia.