11. Yonathani akamjibu, “Njoo twende shambani!” Basi, wakaenda.
12. Yonathani akamwambia Daudi, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, na awe shahidi yetu. Kesho au kesho kutwa, wakati kama huu nitamwuliza baba yangu. Ikiwa msimamo wake juu yako ni mzuri nitakueleza.
13. Mwenyezi-Mungu na aniue ikiwa Shauli anakusudia kukudhuru, nami nisikutahadharishe ili uende mahali mbali ambapo utakuwa salama. Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14. Ikiwa nitaendelea kuwa hai basi, nioneshe ule upendo thabiti wa Mwenyezi-Mungu, ili nisife,
15. tena usiache kuitendea jamaa yangu kwa uaminifu milele. Na Mwenyezi-Mungu atakapowakatilia mbali adui zako kutoka duniani,
16. naomba na jina langu lisikatiliwe mbali kutoka jamaa yako. Mwenyezi-Mungu awalipize kisasi adui zako.”