4. Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.
5. Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku za Uzia, mfalme wa Yuda; na BWANA, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.
6. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;
7. lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na BWANA; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru.
8. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba maji yaliyo hai yatatoka katika Yerusalemu; nusu yake itakwenda upande wa bahari ya mashariki, na nusu yake upande wa bahari ya magharibi; wakati wa hari na wakati wa baridi itakuwa hivi.
9. Naye BWANA atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo BWANA atakuwa mmoja, na jina lake moja.
10. Nchi yote itageuzwa kuwa kama Araba, toka Geba mpaka Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu; naye atainuliwa juu, atakaa mahali pake mwenyewe, toka lango la Benyamini mpaka mahali pa lango la kwanza, mpaka lango la pembeni; tena toka mnara wa Hananeli mpaka mashinikizo ya mfalme.
11. Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena; lakini Yerusalemu utakaa salama.
12. Na hii ndiyo tauni, ambayo BWANA atawapiga watu wote waliofanya vita juu ya Yerusalemu; nyama ya mwili wao itaharibika, wasimamapo juu ya miguu yao, na macho yao yataharibika ndani ya vichwa vyao, na ndimi zao zitaharibika vinywani mwao.