Zek. 14:13-21 Swahili Union Version (SUV)

13. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba mashaka makubwa yatokayo kwa BWANA yatakuwa kati yao; na kila mmoja wao atakamata mkono wa jirani yake, na mkono wake utainuliwa ili kushindana na mkono wa jirani yake.

14. Yuda naye atafanya vita juu ya Yerusalemu; na huo utajiri wa mataifa wa pande zote utakusanyika, dhahabu, na fedha, na mavazi; vitu vingi sana.

15. Na hivyo ndivyo itakavyokuwa tauni ya farasi, na nyumbu, na ngamia, na punda, na ya hao wanyama wote watakaokuwamo matuoni mle, kama tauni hiyo.

16. Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, na kuishika sikukuu ya Vibanda.

17. Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, mvua haitanyesha kwao.

18. Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo BWANA atawapiga mataifa, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.

19. Hii ndiyo adhabu ya Misri, na adhabu ya mataifa yote, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.

20. Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA BWANA; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya BWANA vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu.

21. Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa BWANA wa majeshi; nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake; wala siku hiyo hatakuwamo tena mfanya biashara ndani ya nyumba ya BWANA wa majeshi.

Zek. 14