1. Ufunuo wa neno la BWANA juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo BWANA, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake.
2. Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu.
3. Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake.
4. Katika siku hiyo, asema BWANA, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hizo kabila za watu.