1. Ee BWANA, Mungu wa kisasi,Mungu wa kisasi, uangaze,
2. Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze,Uwape wenye kiburi stahili zao.
3. BWANA, hata lini wasio haki,Hata lini wasio haki watashangilia?
4. Je! Wote watendao uovu watatoa maneno,Na kusema majivuno, na kufanya kiburi?
5. Ee BWANA, wanawaseta watu wako;Wanautesa urithi wako;
6. Wanamwua mjane na mgeni;Wanawafisha yatima.
7. Nao husema, BWANA haoni;Mungu wa Yakobo hafikiri.
8. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini;Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?
9. Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?Aliyelifanya jicho asione?
10. Awaadibuye mataifa asikemee?Amfundishaye mwanadamu asijue?
11. BWANA anajua mawazo ya mwanadamu,Ya kuwa ni ubatili.
12. Ee BWANA, heri mtu yule umwadibuye,Na kumfundisha kwa sheria yako;
13. Upate kumstarehesha siku za mabaya,Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.
14. Kwa kuwa BWANA hatawatupa watu wake,Wala hutauacha urithi wake,
15. Maana hukumu itairejea haki,Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.