Zab. 89:26-44 Swahili Union Version (SUV)

26. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

27. Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.

28. Hata milele nitamwekea fadhili zangu,Na agano langu litafanyika amini kwake.

29. Wazao wake nao nitawadumisha milele,Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.

30. Wanawe wakiiacha sheria yangu,Wasiende katika hukumu zangu,

31. Wakizihalifu amri zangu,Wasiyashike maagizo yangu,

32. Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo,Na uovu wao kwa mapigo.

33. Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye,Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo.

34. Mimi sitalihalifu agano langu,Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.

35. Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu,Hakika sitamwambia Daudi uongo,

36. Wazao wake watadumu milele,Na kiti chake kitakuwa kama jua mbele zangu.

37. Kitathibitika milele kama mwezi;Shahidi aliye mbinguni mwaminifu.

38. Walakini Wewe umemtupa na kumkataa,Umemghadhibikia masihi wako.

39. Umechukizwa na agano la mtumishi wako,Umeinajisi taji yake na kuitupa chini.

40. Umeyabomoa maboma yake yote,Umezifanya ngome zake kuwa magofu.

41. Wote wapitao njiani wanateka mali zake;Amekuwa laumu kwa jirani zake;

42. Umeutukuza mkono wa kuume wa watesi wake;Umewafurahisha wote wanaomchukia.

43. Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake;Wala hukumsimamisha vitani.

44. Umeikomesha fahari yake;Kiti chake cha enzi umekitupa chini.

Zab. 89