Zab. 22:17-30 Swahili Union Version (SUV)

17. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote;Wao wananitazama na kunikodolea macho.

18. Wanagawanya nguo zangu,Na vazi langu wanalipigia kura.

19. Nawe, BWANA, usiwe mbali,Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.

20. Uniponye nafsi yangu na upanga,Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.

21. Kinywani mwa simba uniokoe;Naam, toka pembe za nyati umenijibu.

22. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,Katikati ya kusanyiko nitakusifu.

23. Ninyi mnaomcha BWANA, msifuni,Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni,Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.

24. Maana hakulidharau teso la mteswa,Wala hakuchukizwa nalo;Wala hakumficha uso wake,Bali alipomlilia akamsikia.

25. Kwako zinatoka sifa zanguKatika kusanyiko kubwa.Nitaziondoa nadhiri zanguMbele yao wamchao.

26. Wapole watakula na kushiba,Wamtafutao BWANA watamsifu;Mioyo yenu na iishi milele.

27. Miisho yote ya dunia itakumbuka,Na watu watamrejea BWANA;Jamaa zote za mataifa watamsujudia.

28. Maana ufalme una BWANA,Naye ndiye awatawalaye mataifa.

29. Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,Humwinamia wote washukao mavumbini;Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,

30. Wazao wake watamtumikia.Zitasimuliwa habari za BWANA,Kwa kizazi kitakachokuja,

Zab. 22