Zab. 119:36-51 Swahili Union Version (SUV)

36. Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako,Wala usiielekee tamaa.

37. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa,Unihuishe katika njia yako.

38. Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako,Inayohusu kicho chako.

39. Uniondolee laumu niiogopayo,Maana hukumu zako ni njema.

40. Tazama, nimeyatamani mausia yako,Unihuishe kwa haki yako.

41. Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi,Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.

42. Nami nitamjibu neno anilaumuye,Kwa maana nalitumainia neno lako.

43. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe,Maana nimezingojea hukumu zako.

44. Nami nitaitii sheria yako daima,Naam, milele na milele.

45. Nami nitakwenda panapo nafasi,Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.

46. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme,Wala sitaona aibu.

47. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,Ambayo nimeyapenda.

48. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda,Nami nitazitafakari amri zako.

49. Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako,Kwa sababu umenitumainisha.

50. Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu,Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.

51. Wenye kiburi wamenidharau mno,Sikujiepusha na sheria zako.

Zab. 119