21. Umewakemea wenye kiburi,Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
22. Uniondolee laumu na dharau,Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
23. Wakuu nao waliketi wakaninena,Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
24. Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,Na washauri wangu.
25. Nafsi yangu imeambatana na mavumbi,Unihuishe sawasawa na neno lako.
26. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,Unifundishe amri zako.
27. Unifahamishe njia ya mausia yako,Nami nitayatafakari maajabu yako.
28. Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito,Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
29. Uniondolee njia ya uongo,Unineemeshe kwa sheria yako.
30. Nimeichagua njia ya uaminifu,Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
31. Nimeambatana na shuhuda zako,Ee BWANA, usiniaibishe.
32. Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako,Utakaponikunjua moyo wangu.
33. Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako,Nami nitaishika hata mwisho.
34. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
35. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,Kwa maana nimependezwa nayo.