11. Maji yakawafunika watesi wao,Hakusalia hata mmoja wao.
12. Ndipo walipoyaamini maneno yake,Waliziimba sifa zake.
13. Wakayasahau matendo yake kwa haraka,Hawakulingojea shauri lake.
14. Bali walitamani sana jangwani,Wakamjaribu Mungu nyikani.
15. Akawapa walichomtaka,Akawakondesha roho zao.
16. Wakamhusudu Musa matuoni,Na Haruni, mtakatifu wa BWANA.
17. Nchi ikapasuka ikammeza Dathani,Ikaufunika mkutano wa Abiramu.
18. Moto ukawaka katika mkutano wao,Miali yake ikawateketeza wabaya.
19. Walifanya ndama huko Horebu,Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
20. Wakaubadili utukufu waoKuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
21. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,Aliyetenda makuu katika Misri.
22. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
23. Akasema ya kuwa atawaangamizaKama Musa, mteule wake, asingalisimama,Mbele zake kama mahali palipobomoka,Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.