Zab. 105:23-40 Swahili Union Version (SUV)

23. Israeli naye akaingia Misri,Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.

24. Akawajalia watu wake wazae sana,Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao.

25. Akawageuza moyo wawachukie watu wake,Wakawatendea hila watumishi wake.

26. Akamtuma Musa, mtumishi wake,Na Haruni ambaye amemchagua.

27. Akaweka mambo ya ishara zake kati yao,Na miujiza katika nchi ya Hamu.

28. Alituma giza, kukafunga giza,Wala hawakuyaasi maneno yake.

29. Aliyageuza maji yao yakawa damu,Akawafisha samaki wao.

30. Nchi yao ilijaa vyura,Vyumbani mwa wafalme wao.

31. Alisema, kukaja makundi ya mainzi,Na chawa mipakani mwao mwote.

32. Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe,Na moto wa miali katika nchi yao.

33. Akaipiga mizabibu yao na mitini yao,Akaivunja miti ya mipaka yao.

34. Alisema, kukaja nzige,Na tunutu wasiohesabika;

35. Wakaila miche yote ya nchi yao,Wakayala matunda ya ardhi yao.

36. Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi,Malimbuko ya nguvu zao.

37. Akawatoa hali wana fedha na dhahabu,Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa.

38. Misri ilifurahi walipoondoka,Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia.

39. Alitandaza wingu liwe funiko,Na moto utoe nuru usiku.

40. Walipotaka akaleta kware,Akawashibisha chakula cha mbinguni.

Zab. 105